Mama Mzazi wa mwenyekiti mstaafu Kijiji na Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, wilaya na Mkoa wa Lindi, Mwanahawa Abdallah (65) inaelezwa amekufa baada ya kusombwa na maji alipokuwa anaoga kwenye mto Lukuledi.

Library Photo

Na Mwandishi Wetu

Kwa mujibu wa taarifa kutokea kijijini humo na kuthibitishwa na familia wakiwemo watoto watatu wa marehemu Rashidi Mega, Mwajuma Mega, Sadamu Huseni na kiongozi wa Serikali wa Kata hiyo, inaeleza kuwa, Mwanahawa amekutwa na mkasa huo, Januari 20, 2023 saa 8:00 mchana.

Mtoto wa mwisho wa marehemu Rashidi Mega akielezea tatizo hilo kwa niaba ya wenzake amesema, siku hiyo mama yao aliongozana na Fatuma Dadi ambaye ni jirani yao kuelekea Shambani na walipofika katika mto huo, mama yao alimueleza msanjari mwenzake amsubiri anakwenda kunawa maji.

Amesema baada ya kuona muda unaenda Fatuma aliamua kumfuata mama yao huko mtoni kwa lengo la kumuhimiza waondoke kuelekea nyumbani na alipofika alikuta nguo na mboga ya majani aliyokuwa amebeba (mchicha na kisamvu) hali iliyomlazimu kuanza kumuita lakini hakujibiwa.

Amesema kutokana na hali hiyo jirani yao alirejea Nyumbani na kutoa taarifa kwa watoto wake, ambao nao waliwaambia wanakijiji wenzao na ilipofika saa 9:00 alasiri waliondoka kuelekea mto Lukuledi kumtafuta mama yao, kazi iliyofanyika kwa siku mbili mfululizo bila kufanikiwa.

“Ule mto unafahamika kuwa na mamba wengi, tukafahamu mama yetu ameshachukuliwa na wanyama hao” Alisema Rashidi.

Rashidi aliyewahi kushika nafasi ya mwenyekiti wa Kijiji cha Kiwalala, kwa vipindi viwili vya miaka kumi mfululizo, anasema siku hiyo walimtafuta hadi saa 1:00 usiku bila ya kumuona. Walirejea tena siku ya pili yake, huku idadi ya watu ikiongezeka katika zoezi la kumtafuta na mara zote hawakufanikiwa kumuona.

‘’Siku iliyofuata wana kijiji zaidi ya 80 walituunga mkono kwenda kumtafuta tena japo tuambulie kupata mwili wa mama yetu hatukumuona” Alisema Rashidi Mega.

Naye, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiwalala, Zaituni Chilinga amekiri kupotea kwa Mwanahawa Abdallah tarehe 20 Januari 2023 na mwili wake umepatikana siku ya tarehe 23 Januari 2023. 

Taarifa ya kupatikana mwili huo inatolewa na Mwananchi ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe kuwa mnamo saa 8 mchana siku ya Jumatatu mkulima mmoja mkazi wa Ruo aliuona mwili huo na kutoa taarifa kwa kupiga simu kwa wakazi wa kiijiji cha Kiwalala ambao walifika eneo la tukio Pamoja na ndugu wa marehemu walioridhia kuuzika mwili pasi na kurejea nao nyumbani kwani ulikuwa umeharibika na kuanza kushambuliwa na wadudu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pili Mande alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alijibu bado haijaweza kumfikia na kueleza kuwa, atawatuma vijana wake kufuatilia hali hiyo ili Ofisi yake iwe na taarifa na kufanya uchunguzi wake.

Post a Comment

Previous Post Next Post