Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga ametoa siku tatu kuanzia jana Januari 25 hadi 27 kwa watendaji wa kata Wilayani humo kupita nyumba kwa nyumba kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza  wanakwenda shuleni ifikapo Jumatatu Januari 30, 2023.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga

Na Elizabeth Msagula

Ndemanga ametoa agizo hilo Januari 25, 2023  katika kikao kazi cha wadau wa elimu kilichoshirikisha maafisa elimu msingi na Sekondari, maafisa tarafa, watendaji wa kata, vijiji na Wilaya.

Ndemanga amesikitishwa na hali ya uripoti wa wanafunzi wa kidato cha kwanza katika halmashauri zilizopo kwenye wilaya hiyo ambapo amesema kwa Halmashauri ya Mtama, walioingia darasani hadi kufikia Januari 19 ni asilimia 36 tu ya watoto wote waliotakiwa kuripoti huku zaidi ya asilimia 64 wakiwa hawajaripoti ambao ni watoto 1808 kati ya 2836.

Kwa upande wa halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambao hawajaripoti kidato cha kwanza ni karibu 28% huku walioripoti ni wanafunzi 2203 kati ya 3231. Ndemanga ametumia nafasi hiyo pia kuwaeleza wazazi kuwa sare isiwe kigezo cha kukaa na watoto nyumbani.


Awali, afisa elimu sekondari Manispaa ya Lindi Rehema Makiwa Nahale amesema kuna mpango mkakati kwa kila mkuu wa idara kupangiwa kata ya kwenda kusaidiana na watendaji wa kata wakipita nyumba kwa nyumba kuhakikisha watoto wote wanaripoti shuleni.

Post a Comment

Previous Post Next Post