Taasisi inayoshughulikia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Ruvuma na nchini kwa ujumla, Ruvuma Orphanage Association (ROA), imezishauri shule za awali kuhakikisha zinashirikiana na Serikali ili kuufahamu na kuutekeleza kikamilifu Mpango wa MTAKUWWA, unaolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuimarisha malezi na makuzi bora.


Na Stella Ngenje – Songea

Hayo yamesemwa tarehe 15 Novemba 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa ROA, Bw. Matthew Ngalimanayo, wakati wa mahafali ya kwanza ya Cheers Daycare Center yaliyofanyika katika eneo la Mahenge, Manispaa ya Songea. Akiwa mgeni rasmi, alisisitiza kuwa mpango wa MTAKUWWA ni muhimu kwa sababu unatoa elimu ya malezi yenye mwitikio kupitia ujifunzaji wa awali.

Akihutubia hadhira, Ngalimanayo alisema: “Nawaomba Cheers Daycare Center tuwe karibu na Serikali ili tuujue vizuri mpango huu. Ujifunzaji wa awali ni muhimu sana kwa mtoto. Pia kuna suala la lishe bora. Sambamba na hayo nawaomba sana wazazi na walezi muongozane na watoto wenu kwenda nyumba za ibada ili kuwajenga kiroho, kwa kuwa elimu hii hujengwa kwa vitendo.”

Akiwapongeza wazazi wanaochangia gharama za uendeshaji wa shule hiyo bila kusababisha usumbufu, Mkurugenzi huyo alisema uwajibikaji wao unawajengea walimu moyo wa upendo na ufanisi katika kuwalea na kuwafundisha watoto wenye umri wa miaka 0–8. Alifafanua pia tafsiri ya mtoto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inayomtambua mtoto kuwa ni mtu chini ya miaka 18, akisisitiza umuhimu wa malezi kwa makundi ya umri wa miaka 0–8 ambako ukuaji wa ubongo hukua kwa kasi.

“Mtoto anapozaliwa ubongo huwa umejengeka kwa asilimia 25, na akifikia miaka 6 unakuwa umejengeka kwa asilimia 90. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika malezi na makuzi yao. Wazazi acheni kuwatukana watoto kwa kuwa wanajifunza kwa vitendo,” alisisitiza.

Aidha, Ngalimanayo aliushauri uongozi wa Cheers Daycare Center kutafuta taarifa zaidi kuhusu MTAKUWWA na kumuomba Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Songea, Bi. Edda Venant Komba, kuwa walezi wa shule hiyo ili kuiunganisha na mipango mbalimbali ya Serikali.

Kwa upande wake, mwanzilishi na mmiliki wa shule hiyo chini ya Kanisa la Pentecostal Holiness Mission (PHM), Mwl. Shadrack Mwera, alisema Cheers Daycare Center ilianza mwaka 2024 ikiwa na wanafunzi wawili tu, lakini hadi 2025 imefikia wanafunzi 30, walimu 2 na mpishi mmoja. Alibainisha changamoto ya uhaba wa eneo la kufundishia na kuomba wadau kumsaidia kupatikana kwa kiwanja cha kujenga shule.

Katika risala ya wahitimu iliyosomwa na mtoto Doreen Stanley Mrema, wahitimu walieleza changamoto za uhaba wa madarasa, madawati na vifaa vya michezo, risala iliyogusa mioyo ya waliohudhuria kutokana na ujasiri wa mtoto huyo mdogo mwenye umri wa miaka 5 kuisoma  risala hiyo kwa utulivu na kujiamini.

Akijibu risala hiyo, Ngalimanayo aliahidi kushirikiana na shule kupata eneo la kujenga jengo jipya la shule pamoja na kuchangia ujenzi na mahitaji mengine.

Mchungaji wa kanisa la PHM , Elimu Bernard Mwenzegule, aliwasihi wazazi kuwa makini na malezi ya watoto ili waweze kujitambua, kujithamini, kuwapenda wengine na kumjua Mungu. Aliwapongeza walimu kwa kazi yao kubwa ya kulea na kufundisha watoto, akisisitiza kuwa watoto wajifunze pia kupitia maisha ya wazazi wao.

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Songea Bi. Edda Venant Komba, aliwahimiza wazazi kusimamia mienendo ya watoto na kuwaongoza kwa upendo bila kuwaumiza kisaikolojia. Alisisitiza kuwa kumuonya mtoto ni muhimu, lakini kushindwa kufanikisha jambo kwa mzazi, si vizuri kumweleza mtoto kwa kuwa inaathari kisaikolojia. 

Naye Sajenti Tuntufye Daimon Kabila kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Songea, aliwasisitiza wazazi kuweka kanuni na mipaka kwa watoto na kuwa mfano bora. “Ukimfundisha mtoto uwajibikaji na kumpa upendo bila masharti, unamjenga kuwa na upendo, kujiamini na kujithamini,” Pia aliwasihi wazazi kujikagua na kurekebisha mienendo yao wanapolea watoto.

Wazazi wameushukuru uongozi wa Cheers Daycare Center kwa malezi bora, maadili mema na elimu yenye ubora, wakisema shule hiyo imekuwa nguzo muhimu katika kuwajenga watoto wao kimaadili, kiakili na kitabia.

Post a Comment

Previous Post Next Post