Wakazi wa halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi wameshukuru kwa hatua ya Serikali kupitia wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuanza Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Mtama - Lihima yenye urefu wa mita 800. 


Na Elizabeth Msagula

Barabara hiyo imewekewa jiwe la msingi leo Aprili 11, 2023 na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdallah Shaib Kaim na ujenzi wake unagharimu kiasi cha shilingi Milioni 469 za mfuko wa jimbo. Wakazi hao kutoka vijiji vya Lihimba, Majengo A na B wamesema barabara hiyo pindi itakapokamilika itawasaidia kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka mashambani hadi sokoni.

Naye Waziri wa habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari ambaye pia ni Mbunge wa Mtama amesema barabara ya Lihimba itakuwa mkombozi kwa wakazi hao. Awali akisoma taarifa juu ya ujenzi wa mradi huo wa barabara, Meneja wa TARURA Wilaya ya Lindi Mhandisi Dawson Paschal amesema ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 52 na kwamba inajengwa na Mkandarasi Suma Jkt Construction Ltd. Ameeleza kwamba ujenzi ulianza Juni 20, 2022 na unatarajiwa kukamilika Juni 20, 2023 ambapo itaunganisha wakazi wa vijiji vitatu vya Lihimba, Majengo A na B. 


Naye Mkimbiza Mwenge wa uhuru Kitaifa 2023 Abdallah Shaib Kaim amewahimiza wasimamizi wa mradi ambao ni TARURA kumsimamia vyema mkandarasi ili aweze kukamilisha barabara hiyo kwa wakati uliopangwa kwenye mkataba.  


Kwa halmashauri ya Mtama, Mwenge wa uhuru umezindua mfumo wa TEHAMA hospitali ya Nyangao, utoaji wa huduma za lishe shule ya msingi Mbalala, umeweka pia jiwe la msingi ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa shule ya msingi Songambele - Nyengedi na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa tenki la Maji Mtama.

Post a Comment

Previous Post Next Post