Kukamilika kwa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari Milola iliyopo manispaa ya Lindi kunatajwa kuanza kuleta mabadiliko chanya. Hiyo ni baada ya shule hiyo kupata mwanafunzi wa kike aliyefaulu kwa daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2022 ikiwa ni mara ya kwanza tangu shule hiyo ianzishwe.  


Na Elizabeth Msagula 

Bweni hilo lililojengwa kwa ushirikiano kati ya chuo kikuu cha jimbo la Michigan, Chuo kikuu cha Dar es Salam, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine. Mkuu wa shule ya sekondari Milola Kaimu Maulid Ali akiwa katika hafla ya ufunguzi wa bweni hilo amesema awali wanafunzi wa kike walikuwa wanapata changamoto ya kutembea umbali wa takribani km 20 kutoka kwenye vijiji wanavyoishi hali iliyokuwa inasababisha wengi wao kuacha masomo na wengine kupata ujauzito. 


Baadhi ya wanafunzi walioanza kutumia bweni hilo akiwemo Salama Omari ambaye amepata daraja la kwanza kwenye mitihani ya kidato cha nne licha ya kushukuru, wameomba kuongezewa jengo lingine ili kuwapa nafasi wanafunzi wengine kwani kwa sasa jingo hilo lina uwezo wa kubeba wanafunzi 72 na mahitaji yakiwa ni makubwa zaidi. 

Awali, Prof. Joel Norbet Kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema malengo ya mradi huo walioufanya katika shule ya sekondari Milola ni kufanya kazi na wananchi ili waweze kuwa na maendeleo ambapo kwa ujenzi wa bweni hilo kutasaidia wanafunzi wa kike kutimiza ndoto zao.
 

Naye mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa manispaa Juma Mnwele amehimiza kutunzwa kwa miundombinu iliyowekezwa shuleni hapo.

Post a Comment

Previous Post Next Post