Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema juhudi za kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto katika zama za utandawazi zinahitaji msukumo mpya na wa pamoja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene

Na WMJJWM, Dodoma

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo wakati akiongoza Mkutano wa kupitia tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/18 - 2021/22 (MTAKUWWA) uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa St. Gaspar Jijini Dodoma Januari 26, 2023.

Amebainisha kwamba, athari za utandawazi zimedhoofisha mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto hivyo kufanya kundi hilo kutokuwa salama kwani tatizo la ukatili bado ni changamoto katika ngazi zote.

"Kutokana na changamoto hiyo, Wadau wote tuna wajibu wa kuchukua hatua za kudhibiti na kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yote ikiwemo shuleni na nje ya shule. Changamoto yoyote inayoathiri ukuaji wa wa watoto, inachangia kuandaa nguvu kazi dhaifu isiyokuwa na tija kwa Jamii". amesema Simbachawene.


Ameongeza pia kundi la watoto ni kubwa nchini ambapo ni asilimia 49.06 hivyo linahitaji uangalizi mkubwa katika mfumo mzima wa malezi, makuzi na Maendeleo yao. 

Aidha, Simbachawene ametoa wito kwa Wadau kuwa wavumilivu na kuwahakikishia kuwa, katika mkutano wa Mawaziri ujao ambao utapitisha rasimu ya MTAKUWWA II, utazingatia sana maoni ya wadau.


Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsiia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha kuwa taarifa ya tathmini ya MTAKUWWA  imekamilika na imeainisha maeneo muhimu yanayopendekezwa kutekelezwa kwa mpango ujao, hivyo kikao hicho kinalenga kuipitia na kuboresha ili kuongeza ufanisi.

"Nawaomba Wadau wote kuwa na subira wakati majadiliano ya tathmini yakiendelea kwani wote tunajenga nyumba moja" amesisitiza Waziri Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsiia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Wizara  yake imejipanga kuhakikisha watoto wanapata haki na kwamba tayari mchakato wa kubadili sheria ya ndoa unaendelea kwa kushirikisha wadau wote na mjadala wa mila na desturi kukinzana na ukatili ukiwa umeanza.

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la ICS Tanzania Bw.  Kudely amesema katika kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa kuotokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto, Wadau wameshiriki katika maeneo yote nane kwa kutumia mbinu mbalimbali jumuishi kwa kushirikiana na Wizara za kisekta. 

Post a Comment

Previous Post Next Post