Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Deus Mwakajegele, askari wa uhifadhi aliyekuwa akifanya kazi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambaye alichomwa mshale wenye sumu wakati akitekeleza majukumu yake katika eneo la Nyanungu, wilaya Tarime mkoani Mara.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akitoa pole kwa Mke wa marehemu Deus Mwakajegele, (kushoto) wakiwa na Mama Mzazi wa  askari wa uhifadhi huku akimuangalia mtoto mchanga  aliyeachwa na Marehemu huyo wakati alipofika nyumbani leo katika kijiji cha Ngongongale wilayani Arumeru kwa ajili ya kutoa pole kwa familia iliyompoteza Askari huyo 

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa salamu hizo jana Alhamisi Januari 26, 2023 alipofika nyumbani kwa marehemu eneo la Ngongongale wilayani Arumeru mkoani Arusha kufuatia kuguswa na kifo cha askari huyo ambaye enzi za uhai wake alijitoa kulinda wanyamapori kwa niaba ya Watanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akizungumza na kutoa pole kwa Mjomba  wa marehemu Deus Mwakajegele, mara baada ya kutoa pole kwa wafiwa wakati alipowasili nyumbani leo katika kijiji cha Ngongongale wilayani Arumeru kwa ajili ya kutoa pole kwa familia iliyompoteza Askari huyo

''Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii nimekuja hapa kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Jumuiya yote ya Wahifadhi. Nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kijana wetu aliyeshambuliwa kwa kupigwa mshale wenye sumu na watu wasiojulikana siku ya Jumamosi tarehe 21, 2023 wakati akitekeleza majukumu yake” ameeleza Dkt. Pindi Chana.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akiweka shada la maua katika kaburi la Marehemu Deus Mwakajegele mara baada ya kutoa pole kwa wafiwa wakati alipowasili nyumbani kwa Marehemu leo katika kijiji cha Ngongongale wilayani Arumeru kwa ajili ya kutoa pole kwa familia iliyompoteza Askari huyo 

Kufuatia hali hiyo, Waziri Balozi Dkt.Pindi ametumia fursa hiyo kukemea vikali vitendo  vya baadhi ya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi huku akisisitiza kuwa Jeshi la Uhifadhi liko imara na litaendelea kulinda maeneo yote ya Hifadhi kwa faida na manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Katika hatua nyingine Waziri Chana amebainisha kuwa mtu aliyehusika na tukio lililosababisha kifo cha askari huyo tayari ameshamakatwa huku wengine waliohusika  na tukio hilo wakiendelea kusakwa ili sharia ichukue mkondo wake. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akizungumza na vyombo vya habari  marehemu Deus Mwakajegele, mara baada ya kutoa pole kwa wafiwa wakati alipowasili nyumbani kwa Marehemu  leo katika kijiji cha Ngongongale wilayani Arumeru kwa ajili ya kutoa pole kwa familia iliyompoteza Askari huyo

Kwa upande wake Mjomba wa Marehemu Bw. Sisito Kigongo ameeleza kuwa askari huyo alikuwa ni mhimili kwa familia hivyo kifo chake kimekuwa pigo kubwa kwa  familia huku akibainisha kuwa marehemu ameacha watoto watatu.

Post a Comment

Previous Post Next Post