Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Mhe. Zainab Katimba ametoa rai kwa wanafunzi wote nchini kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufaulu kwa viwango vya juu ili badae walitumikie taifa.
Na Angela Msimbira, GEITA
Mhe.Katimba ametoa rai hiyo alipotembelea shule mpya maalum ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita kwa lengo la kukagua miundombinu iliyojengwa na kujionea maboresho yaliyofanywa na serikali katika ujifunzaji na ufundishaji kwenye sekta ya elimu nchini.
Amesema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu iliyobora katika mazingira mazuri hivyo ni wajibu wa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.
“Namna pekee ya kumlipa Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha na kujenga miundombinu iliyobora na kuhakikisha mnapata elimu bila ada ni kuhakikisha na ninyi mnasoma kwa bidii, mfaulu vizuri na kupata elimu bora ili baadaye muweze kulitumikia taifa.”
Katimba amesema wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa Taifa linawategemea, hivyo amewataka kuhakikisha hawafanyi mchezo wakiwa shuleni bali watumie fursa hiyo kujenga kesho yao.
Akitoa taarifa ya elimu Mkoa wa Geita, Katibu Tawala Mkoa huo, Mohamed Gombati amesema kwa upande wa shule ya sekondari ya wasichana imepokea Sh bilioni 3 katika awamu ya kwanza na Juni mwaka huu zimepokelewa Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo na tayari imeshaanza kuchukua wanafunzi.
Amesema kwa mwaka 2021/22 Mkoa wa Geita ilipokea Sh bilioni 17, mwaka 2022/23 zilipokelewa Sh bilioni 31 na kwa mwaka 2023/24 zilipokelewa Sh bilioni 32 bila kujumuisha fedha zinazotolewa kugharamia elimu bila ada.
Amesema kuwa katika fedha za ndani zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo za asilimia 60 au 40 kiwango kikubwa kinaelekezwa kwenye sekta ya elimu.
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita, Mwamin Kagoma amesema shule hiyo imegharimu Sh bilioni 4 na mpaka sasa wanafunzi 172 kati ya 211 waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano wameripoti shuleni.
Post a Comment