NIRC Iringa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imesema imeridhishwa na matumizi ya fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya umwagiliaji nchini na kuitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kutekeleza azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula.


Akizungumza wakati kamati hiyo ikihitimisha ziara ya kukagua miradi ya umwagiliaji katika mradi wa umwagiliaji wa Mkombozi uliopo tarafa ya Pawaga mkoani Iringa, Mwenyekiti wa kamati hiyo Daniel Sillo amesema kamati imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizofikiwa utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji hivyo kukamilika kwa miradi hiyo italeta tija katika sekta ya kilimo na kuinua pato la Taifa.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde amesema serikali imedhamiria kupeleka miundombinu ya umwagiliaji maeneo yote yanayofaa kwa kilimo ikiwemo ujenzi wa mabwawa na skimu.

 

Amesema mikakati iliyopo katika miradi yote ya umwagiliaji serikali inajenga barabara lengo kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani na kuhakikisha mazao hayapotei shambani kutokana na miundombinu mibovu ya barabara.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amesema miradi yote 48 inayotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 inaendelea vizuri na matarajio itakamilika kwa muda uliopangwa.

 

Aidha akizungumzia mradi ujenzi skimu ya umwagiliaji Mkombozi amesema ni mradi mkubwa wenye hekta 6,000 unahusisha vijiji sita, thamani yake ni shilingi bilioni 55 ambapo wananchi watakaonufaika ni 16,000.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilitembelea miradi ya umwagiliaji katika mkoa wa Dodoma, Arusha, Manyara Singida na kuhitimisha ziara hiyo ya ukaguzi miradi ya umwagiliaji mkoani Iringa.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post