Kutokana na umuhimu wa Mazoezi ya mwili  kwa binadamu  ikiwemo kusaidia katika kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo kiwango cha sukari mwilini,  pamoja na kupunguza uzito wa mwili, jamii imeaswa kujenga mazoea ya ya kufanya mazoezi mara kwa mara.

Na. Elimu ya Afya kwa Umma

Hayo yamejiri   Jijini Dodoma  katika Utekelezaji wa Mpango wa Mazoezi na Afya ya Mwili kwa watumishi ndani ya Idara ya Kinga ambapo watumishi wa idara hiyo wamekuwa na mpango wa kufanya mazoezi kila Jumatatu katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma  na kila Jumatano na Ijumaa katika uwanja wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Afya Mazingira , Wizara ya Afya Dkt.Khalid Massa amesema mazoezi hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha Kinga dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza.

“Tukiwa  katika Wiki hii ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza  iliyoanza Novemba 11 hadi 18, 2023 tumeendelea na mazoezi hivyo ni vyema viongozi na watu wote tukaendelea kujumuika na mazoezi haya ni fiti yana umuhimu kuzuia  magonjwa yasiyoambukiza” amesema  Dkt.Khalid Massa Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Afya Mazingira, Wizara ya Afya .

Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu   ya Ufuatiliaji wa Magonjwa na Epidemiolojia Wizara ya Afya Dkt.Vida Mbaga amesema mazoezi husaidia kupunguza uzito na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini huku Asteria Shirima kutoka sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma akisema elimu ya afya ikiwemo lishe bora na umuhimu wa mazoezi imekuwa ikitolewa kwa jamii inayohudhuria katika mazoezi hayo.

Ikumbukwe kuwa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya  imeanzisha Mpango kwa watumishi kufanya mazoezi mara mbili kwa wiki Jumatano na Ijumaa jioni mara baada ya saa za kazi kuanzia saa 9:30 hadi saa 11:00 jioni hiyo ni katika kuungana na mkakati endelevu wa Wizara ya Afya wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza.

Post a Comment

Previous Post Next Post