Msimbati - Mtwara
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko ameagiza kuondolewa kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na kushindwa kutoa
taarifa mbalimbali na kutofanya mikutano na wananchi wanaozunguka miradi
ya Gesi Asilia ikiwemo dharura zinazotokea katika Mkuza wa Bomba la
Gesi.
Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo tarehe 14 Novemba, 2023
wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa
Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya
kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata
ya Msimbati wilayani humo.
Wananchi wa Kata ya Msimbati
walimweleza Dkt.Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara,
kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa
uchakataji Gesi Asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata
taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba
la Gesi Asilia.
“Changamoto kwenye miradi hii zinatokea lakini
lazima awepo mtu ambaye ni daraja kati ya Serikali na Wananchi, na Mtu
huyu analipwa mshahara kwa kazi hiyo, haiwezekani Waziri au Rais kuja
kutoa taarifa kwa wananchi wakati kuna mtu kaajiriwa kwa kazi husika,
wananchi hawa wanapaswa kupata taarifa.” Amesisitiza Dkt.Biteko
Katika
hatua nyingine, ameagiza Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja katika Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na
majibu yasiyo stahiki wanayojibiwa wananchi wanapopiga simu kwenye
Shirika hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Vilevile,
Dkt. Biteko ameagiza kuwa, miradi inapotekelezwa katika eneo lazima
ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za
kijamii kama vile Shule, Vituo vya Afya, Barabara na Maji.
"Changamoto
zote mlizozieleza hapa nataka niwahakikishie kuwa zitashughulikiwa,
nataka muone tofauti kuanzia sasa, kama Gesi Asilia inatoka hapa na
inaendesha mitambo ya umeme kwa asilimia 65, haiwezekani wala haiingii
akilini, watu hawa wakalia kituo cha Afya, Polisi, ubovu wa barabara,
haiwezekani, nataka niwaeleze kwamba ushuru wa huduma unaokusanywa na
halmashauri sehemu ya fedha lazima irudi hapa." Amesema Dkt. Biteko.
Dkt.
Biteko, amewaagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja Mkuu wa Wilaya kukaa
pamoja na wananchi wa eneo hilo ili mpango wa maendeleo wa kijiji hicho
uandaliwe, hivyo fedha zinapotolewa zifanye maendeleo kulingana na
mpango wa kijiji.
Aidha, ameiagiza TPDC kuweka mpango maalum wa
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Jamii (CSR) katika eneo hilo ili
wananchi hao waone faida ya kuwepo kwa miradi kwenye maeneo yao na
kuwaelekeza kuwaagiza wajenge kituo cha afya, taa za barabarani na Kituo
cha Polisi.
Ili kuhakikisha kuwa, Jamii zinazozunguka na miradi
ya Mafuta na Gesi Asilia zinafaidika na uwepo wa miradi hiyo,
Dkt.Doto.Biteko amesema kuwa Serikali itakuja na kanuni zitakazoongoza
masuala ya CSR lengo likiwa ni kuhakikisha jamii zinazozunguka miradi ya
Mafuta na Gesi zinanufaika.
Post a Comment