Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo nchini (TAUS) pamoja na Daktari Bingwa kutoka Ufaransa kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza uume kwa Watu wawili wenye matatizo ya nguvu za kiume ambao uume ulishindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.
Akiongea baada ya kukamilisha upasuaji Dkt. Remigius Rugakingira Daktari Bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na Wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.
“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyowezesha uume kurudi katika hali yake ya kufanya kazi, upasuaji huu tumeshirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa mfumo wa mkojo pamoja na Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo kutoka Ufaransa na tumefanikiwa katika hilo”
Dkt. Rugakingira amesema huu ni wito kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya Wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania.
Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume.
Post a Comment