YOUR FUTURE IS CREATED BY WHAT YOU DO TODAY, NEVER TOMORROW
Mjadala juu ya bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2023/2024 umeendelea kuchukua sura mpya bungeni jijini Dodoma kila siku ambapo wabunge wamehoji juu ya kuongezeka kwa kodi ambazo zinakwenda kuongeza mzigo kwa wananchi na kuiomba serikali kuunda mfuko wa pembejeo na kinga ya mazao hususani mazao ya kimkakati pindi bei ya masoko inapotikisika.
Akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2023/24, Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amepinga pendekezo la Serikali kuongeza Tsh. 100 kwenye kila Lita ya Dizeli na Petroli kwa maelezo kuwa tayari Mafuta yana Kodi 22.
Akifafanua zaidi amesema, kuna baadhi ya Kodi zinazotozwa kwenye Mafuta zinakwenda kwenye Ujenzi wa Barabara hivyo ongezeko hilo litasababisha nauli za Mabasi na Daladala zipande pamoja na kuongeza gharama nyingine za Maisha. Kuhusu ongezeko la Tsh. 200 kwenye kila Kilo ya Saruji, Gambo amesema Kodi hiyo itamnyima Mtanzania uwezo wa kununua Saruji kwaajili ya ujenzi wa Nyumba nzuri na hivyo Serikali itafute chanzo kingine cha mapato na sio kumbebesha kodi Mwananchi.
Naye mbunge wa viti maalumu Salome Makamba akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jijini Dodoma leo amesema Taifa haliwezi kuendelea kama kutakuwa na mtindo wa kuongeza kodi katika maeneo mbalimbali badala ya kuongeza walipa kodi.
Aidha Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani ameiomba Serikali kuendelea kupunguza kodi zinazowabana wanunuzi wa tumbaku nchini ili wakulima wa zao hilo waendelee kupata faida kubwa.
Pia ameeleza kilio cha wakulima wa pamba nchini wanaouza kwa bei ya chini na kuiomba serikali kuwepo kwa mfuko wa pembejeo na kinga ya mazao hususani mazao ya kimkakati pindi bei ya masoko inapotikisika.
Post a Comment