Wakazi wa kijiji cha Mbute kata ya Namapwia wilayani Nachingwea wameiomba serikali kuingilia kati juu ya mgogoro wa mpaka dhidi ya Kijiji cha Nangulugai kilichopo wilayani Ruangwa kwani unahatarisha usalama na kuwakosesha mapato kupitia msitu wao wa hifadhi ambao umezuiwa kutumika kwa sasa. 


Wakizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama na timu ya wataalamu wa wilaya ya Nachingwea wamesema mgogoro huo umekuwa wa muda mrefu Sasa na haujapatiwa ufumbuzi na unaleta athari kwani kwa sasa hawawezi kuvuna mazao ya msitu wao wa hifadhi wa Chilalo kutokana na zuio la kutoka kwa katibu tawala wa mkoa wa Lindi. 

Pia wakazi hao wamesema wanashangazwa na kuona licha ya zuio hilo la kutotumia msitu huo, bado watu wa kijiji cha Nangulugai kilichopo Ruangwa wanaendelea na shughuli za uvunaji na kilimo katika msitu huo na wanapojaribu kuwakamata wanasema wameruhusiwa na viongozi wa vijiji hivyo kufanya shughuli za kiuzalishaji katika eneo hilo na wakati mwingine wakipokea simu kutoka kwa baadhi ya viongozi kuwasitisha na ukamataji huo, huku wakieleza kuwa  kwa sasa kuna barabara inayochongwa kutoka katika vijiji vya Ruangwa kuingia msituni humo pasipo wao kutambua. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Moyo amewataka wakazi hao kuwa watulivu na kuacha kutumia maneno makali kwa viongozi, huku akieleza kuwa eneo la Chilalo lipo na kuhusu mgogoro wa mpaka kwa sasa upo katika ngazi ya mkoa ila ataendelea kufuatilia ili uweze kupatiwa suluhu.

Post a Comment

Previous Post Next Post