YOUR FUTURE IS CREATED BY WHAT YOU DO TODAY, NEVER TOMORROW
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga ametoa wito kwa Wanajumuiya wa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO's) pamoja na viongozi wa serikali za kata na vijiji kutambua kwa kina taarifa za miradi ya Maji inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao.
Ndemanga ametoa wito huo Leo, Juni 20, 2023 katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO's) unaoratibiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
"Sote tuna Jukumu la kuitambua miradi inayotekelezwa kuanzia ujenzi wake, gharama zake na huduma inayotarajiwa kutolewa na miradi hiyo katika jamii zetu pamoja kuisaidia jamii kuelewa kwa kina kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Usambazwaji wa huduma ya Maji Safi na Salama nchi nzima na hususan katika Wilaya yetu ya Lindi." Ameeleza Ndemanga.
Aidha, Ndemanga amewataka Wanajumuiya hao kutoa hamasa kwa Wananchi katika maeneo yao Kuvuta huduma za maji katika makazi yao wanayoishi ili iweze kuwarahisishia katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuwa wabunifu katika kutumia njia mpya za uboreshaji wa huduma wanazotoa.
Akitoa taarifa ya Hali ya Upatikanaji wa Maji katika Wilaya ya Lindi, Mhandisi. Athanas Lume, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lindi ameeleza kuwa Lengo kuu la RUWASA ni kuhakikisha inatekeleza miradi ya Maji hasa katika maeneo ya vijijini na wananchi wanapata huduma za Maji Safi na Salama.
"Utekelezaji wa Miradi ya RUWASA kwa sasa umefikia 76% ukilinganisha na wakati tunaanza kazi mwaka 2019 ambapo tulikua na 59%, na kwa kasi hii tunayoendelea nayo tunaamini hadi kufikia mwaka 2025 tutafikia lengo la 85% kama ilivyo ilivyohaidiwa katika ilani ya Chama Tawala"
Kwa mwaka wa fedha 2022/23 tumetekeleza jumla ya miradi 6 yenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.676 kwa kutumia mfumo wa Force Account ambapo tumefanya kazi ikiwemo Uboreshaji wa Mradi wa Milola, Utekelezaji wa mradi wa Maji wa Namunda- Mnolela pamoja na Utekelezaji wa Mradi wa Mawilo. Kwa Mwaka ujao wa Fedha unaotarajiwa kuanza Julai, 2023 RUWASA inatarajiwa kutekeleza miradi yenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.69
Post a Comment