Kikosi Maalum cha Wanamgambo nchini Sudan cha RSF, kimesema kimechukua udhibiti kamili wa Ikulu ya rais, makaazi ya mkuu wa jeshi Jenerali ABDEL FATTAH AL-BURHAN na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum.

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumamosi, RSF imesema imechukua pia udhibiti wa viwanja vingine viwili vya ndege, kwenye mji wa kaskazini wa Merowe na mji wa El-Obeid ulioko upande wa kusini mwa nchi.

Kiongozi wa Kikosi Maalum cha Wanamgambo, RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo

Tarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa katika kujibu mashambulizi yanayofanywa na jeshi dhidi ya kambi za RSF kusini mwa mji mkuu, Khartoum.

Awali kikosi cha RSF kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayefahamika zaidi kwa jina la Hemedti, kilisema kuwa jeshi lilizingira moja ya kambi zake na kufyatua risasi kwa kutumia silaha za kivita.

Wakati huo huo, vyama vya kiraia vya Sudan ambavyo vimesaini makubaliano ya awali ya kugawana madaraka na jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi cha RSF vimetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yaliyozuka baina ya vikosi hivyo viwili.

Kwa mujibu wa vyama hivyo pia vimetoa wito kwa wadau wa kimataifa na kikanda kuchukua hatua haraka kuzuia umwagaji damu.


Credit: DW

Post a Comment

Previous Post Next Post