Wazee mkoani Lindi wameomba
kupewa kipaumbele katika maeneo yatolewayo huduma za kijamii ikiwemo hospitali na
wametoa mapendekezo yao ili kuboresha huduma kwa wazee katika jamii ikiwa ni
pamoja na kuundwa kwa sheria itakayotoa adhabu kwa vijana wanaokwepa jukumu la
kuwatunza wazazi wake kipindi cha uzee.
Wameyazungumza hayo katika
kikao cha kwanza cha kamati ya wazee mkoa wa Lindi kilichofanyika leo Februari
14, 2023 katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mganga Mkuu Mkoa wa Lindi, maafisa ustawi wa jamii, wajumbe kutoka timu ya uendeshaji wa huduma za afya mkoa (RHMT), wawakilishi kutoka vyama vya utetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari huku mgeni rasmi katika mkutano huo akiwa ni Dkt. Bora Haule (Phd) ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi - Viwanda, Biashara Na Uwekezaji ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Zainab Telack ambaye amewaomba wazee kuacha kupokea majukumu mazito katika umri wao ikiwemo kuwatunza wajukuu.
Baraza la wazee mkoa wa Lindi
limeanzishwa mwaka 2022 likiwa na lengo la kuwalinda wazee na kuhakikisha wanapata
usimamizi na msaada wa karibu ili kuleta ustawi wa jamii bora kwa kuwa hawana
nguvu tena ya kuhangaika katika nyakati zao za uzee.
Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa
Lindi Dkt. Henry Kyaga ameipongeza serikali kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa
katika kuwalinda na kutambua nafasi ya wazee katika jamii licha ya ukweli
kwamba, katika ngazi ya mkoa bado hawajafika katika kiwango cha ubora katika
kuyatekeleza hayo. Hivyo ametoa wito kwa madiwani katika halmashauri zote
kuyasimamia mabaraza haya ili yawe hai.
Aidha Dkt. Henry Kyaga ameahidi kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuwahudumia wazee ili kuepukana
na changamoto wanazokutana nazo huku akishauri kuhakikisha vikao vya mabaraza
ya wazee vinafanyika katika ngazi za vijiji, kata na wilaya kwani baadhi ya
changamoto zinaweza kutatulika katika hatua hizo.
Post a Comment