Mchezaji maarufu wa michezo ya Nyoka na muuzaji wa dawa za asili za kujikinga na nyoka mkoani Lindi, Bw Japokuwa Masawila amefariki dunia baada ya kugongwa na nyoka ambaye alidhamiria kumdhibiti. 


Mshika nyoka huyo ambaye ni maarufu kama Japo Manyoka, alijeruhiwa na nyoka akiwa katika mapambano makali ya kumdhibiti licha ya kubanwa na nyoka mara kadhaa, awamu hii imekuwa ngumu kwake kunusurika.

Kaimu mganga mfawidhi hospitali ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi (Kinyonga) Dkt Emmanuel Macha amesema nyoka aliemng’ata na kumuua Mtaalam wa tiba asili za nyoka Mkoani Lindi Japokuwa Masawila maarufu ‘Manyoka Nyoka’ Februari 5,2023 anadhaniwa kuwa ni Koboko maaarufu ‘Black Mamba’ ambaye sumu yake huathiri moja kwa moja mishipa ya fahamu. 

Dkt. Macha amesema marehemu huyo alifikishwa hospitalini hapo majira ya saa tatu usiku akiwa na hali mbaya ya kukosa fahamu na kupumua kwa shida.

Ndugu wa karibu wa Marehemu wamesema Japokuwa aliaga kwenda wilayani Kilwa kwaajili ya maonesho yake ya Nyoka ili aweze kuuza dawa za kinga, lakini kwakuwa ni kawaida yake kuweka kambi sehemu na kutafuta nyoka wasumbufu katika maeneo anayofikia, alifanikiwa kupambana na nyoka huyo ambaye alimjeruhi na kumfanya aishiwe nguvu na kumsababishia kifo.

Baada ya Marehemu kuona hali yake kiafya si nzuri, aliwapatia majirani katika eneo hilo Namba ya simu ya mtoto wake pamoja na ya mkewe (mtaliki) ili wajuzwe lakini hawakuwahi kufanya naye mazungumzo zaidi ya kuambiwa tayari ameshafariki.


Naye mwenyekiti wa mtaa katika eneo alilokuwa anaishi mshika nyoka huyo anasema, taarifa ya kufariki kwa Mkazi wake ameipata mapema asubuhi ya leo na kwakuwa Bwana Japo alikuwa na kawaida ya kukaa na Nyoka katika eneo lake la makazi, yeye na viongozi wengine wa serikali wamefanya upekuzi katika chumba alichokuwa anakitumia marehemu kuhifadhi viumbe hao na kwa bahati mazingira yameonekana ni salama.

Majirani, wanasema Japo ni mtu wa ajabu kwani hakuwa akifanana na tabia za wengine walioweza kucheza na nyoka. Alihifadhi nyoka hao kwa siri na mara nyingi alikuwa mcheshi kwa watu wote.

Marehemu anatarajia kuzikwa Nyumbani kwao Mkoani Pwani huku Serikali kupitia ofisi ya Maliasili Mkoani Lindi ikisema, eneo la makazi yake ni salama na hakuna hatari yoyote, lakini mifugo yake haiwezi kurithiwa hivyo itachukuliwa kwaajili ya usalama na kuihifadhi kwani bado ni mali za Asili

Post a Comment

Previous Post Next Post