Imeelezwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Lindi wamekuwa na mwako mkubwa katika uzalishaji wa Mwani ambapo takwimu zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa zao hilo kutoka kilo 993,064 zenye thamani ya shilingi 640,782,400 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia kilo 1,608,770 zenye thamani ya shilingi 927,066,508 kwa mwaka 2021/22.

Afisa uvuvi Mkoa wa Lindi Jumbe Kawambwa

Na Elizabeth Msagula

Afisa uvuvi Mkoa wa Lindi Jumbe Kawambwa amesema hayo katika Mkutano wa wadau wa uvuvi Mkoani Lindi uliofanyika Wilayani Kilwa na kueleza kuwa zao la Mwani linakuwa kwa kasi licha ya kuwepo kwa changamoto ya ubora inayotokana na wakulima kuanika mazao yao chini (ardhini) jambo ambalo linapunguza thamani ya zao hilo katika soko la nje.

Hata hivyo ameweka wazi mikakati ya kushirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi na wadau wengine wa maendeleo na wanatarajia kuanza kuboresha miundombinu ya kukaushia mwani ikiwemo ujenzi wa vichanja katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa kama Songosongo, Mchinga na Mtama ili zao hilo libaki katika thamani yake na kukidhi mahitaji ya soko.

Pia amesema wanao mkakati maalum wa kutoa mafunzo ya kuliongezea thamani zao la mwani kwa vikundi vimavyolima kwa kuanzisha viwanda vidogo ambavyo vitatengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao la mwani, mkakati ambao unatajwa  kuwa utaongeza uzalishaji na mapato na hatimaye kuondokana na kuuza mwani ghafi kwa bei ya chini.

Miongoni mwa wadau katika zao hilo, Mkurugenzi wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali (LANGO), Michael Mwanga ameshauri serikali Mkoani Lindi iangalie utaratibu wa kusimamia vizuri upangaji wa bei katika zao la mwani pamoja na kuangalia utengenezaji wa ushirika katika zao hilo.

Mkurugenzi wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali (LANGO), Michael Mwanga

Post a Comment

Previous Post Next Post