Ujenzi wa wodi ya kisasa ya kujifungulia kina mama wajawazito ulioanza Oktoba 15, 2022 katika zahanati ya Mnali kata ya Kitumbikwela Manispaa ya Lindi umefikia karibu asilimia 70.


Na Elizabeth Msagula

Kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kina mama wa kata hiyo na maeneo jirani waliokuwa wanapata changamoto ya chumba cha kujifungulia ambapo miezi kadhaa iliyopita iliwalazimu kuanza kujenga kibanda cha miti ili kiwasaidie kupata huduma hiyo.

Kibanda cha miti kilichojengwa na wananchi ili kiwasaidie akina mama 
wakati wa kujifungua katika zahanati ya Mnali kata ya Kitumbikwela kabla ya kuanza kwa ujenzi wa wodi ya wazazi

Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Lindi Juma Mnwele amesema wodi hiyo mpya na ya kisasa inayojengwa na serikali kwa kushirikiana na jamii ya watu wa Mnali tayari imeezekwa na halmashauri inatarajia kupeleka tena fedha kiasi cha shilingi Milioni 20 kwa ajili ya kumalizia hatua iliyobaki ya kufunga madirisha, rangi na milango.

Amesema lengo ni wodi hiyo ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa akina mama na kuondokana na changamoto waliyokuwa wanaipata awali na hatimaye wasitirike kwa kupata huduma bora na zenye unafuu. 


Nao Wananchi wa Mnali wameendelea kupongeza ujenzi wa jengo hilo la kisasa maalumu kwa akina mama kujifungulia, ambapo hapo awali wananchi hao walikiri kuchoka kudharirika kutokana na chumba wanachokitumia kuwa kidogo na pia kutumika na wagonjwa wengine.

Post a Comment

Previous Post Next Post