YOUR FUTURE IS CREATED BY WHAT YOU DO TODAY, NEVER TOMORROW


Ruben Ndiza Mfune, Mkuu wa Wilaya ya Mbalali Mkoani Mbeya na Juma Masatu, Mhasibu ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro wakiwasili mahakama ya wilaya ya Ruangwa

Na Elizabeth Msagula

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi imewafikisha mahakamani aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo mwaka 2015-2010 Ruben Ndiza Mfune (58) ambaye kwa sasa ni mkuu wa Wilaya ya Mbalali Mkoani Mbeya na Juma Masatu (56) aliyekuwa mweka hazina katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka 2014 ambaye pia kwa sasa ni  mhasibu ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kuisababishia hasara mamlaka ya zaidi ya Shilingi Mil 51.

Wawili hao wamefikishwa katika mahakama ya  Wilaya ya Ruangwa Januari 11,2023 na kusomewa shauri hilo kwa mara ya kwanza la uhujumu uchumi namba 1, 2023 mbele  ya hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Mariam Mchomba.

Upande wa serikalI, shauri hilo linasimamiwa na wakili Peter Camilius huku upande wa utetezi kukiwa na wakili Sia Ngowi.


Imeelezwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Camilius kuwa mnamo Oktoba 2,2014 washtakiwa walipewa na kupokea fedha kutoka kwa katibu mkuu hazina kiasi cha shilingi Mil 200 zilizowekwa katika akaunti ya maendeleo ya halmashauri kwa ajili ya mradi wa uchimbaji wa visima 11 katika vijiji vya Mtakuja, Ng’alile, Nandanga, Namahema, Namakuku, Likunja, Mbangala, Nandenje, Namilema, Matambalale na Namkaranga.

Katika zoezi hilo kampuni ya uchimbaji ya Maswi ilishinda tenda ya uchimbaji na halmashauri ya Ruangwa ikaingia nao Mkataba kwaajili ya kuanza kazi hiyo kwa malipo ya shilingi 182,740,000/= 

Wakili huyo ameongeza kwa kusema kuwa, Kati ya Oktoba 2 na Disemba 31,2014 washtakiwa walisababisha Mil 192 kutumika kwa matumizi mengine tofauti na yale yaliyokuwa yamepangwa huku halmashauri ikishindwa  kulipa kampuni hiyo ya uchimbaji visima kwa mujibu wa mkataba na hivyo kupitia shauri namba 4,2016 kampuni hiyo iliishitaki halmashauri kwa kuvunja mkataba na Mei 17,2015 kampuni na halmashauri walimaliza Kesi nje ya mahakama ambapo halmashauri ilitakiwa kulipa fidia ya shilingi Mili 200.4

Wakili wa serikali Camilius amesema kesi hiyo ina mashahidi 8 na vielelezo 6 na kwamba  kwa matendo waliyoyafanya ni kinyume na aya ya (10)1 jedwali la 1 na kifungu cha 57(1), 60(2) ya sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 mapitio ya mwaka 2022.

Hata hivyo washtakiwa wamekana hoja hizo za awali zilizotolewa na upande wa jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana endapo washtakiwa watatimiza masharti.

Baada ya kutimiza masharti ya dhamana washtakiwa wapo nje kwa dhamana na februari 7,2023 kesi hiyo itaanza kuskilizwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post