Wananchi wa kata sita zinazounda  wilayani ya Korogwe mkoani Tanga  Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei Na Magila Gereza, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwapelekea mradi wa bwawa la Mkomazi utakaogharimu zaidi shilingi bilioni 18 na kuongeza kuwa ndoto yao ya kusubiri ujenzi wa bwawa hilo kwa zaidi ya miaka 50 sasa imetimia.     



Wakitoa maoni yao wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi baina ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na mkandarasi SICHUAN INTERNATIONAL COOPERATION (SIETCO) ya nchini China, wakazi hao wamesema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa hilo, eneo la kilimo litaongezeka kutokana uwepo wa maji ya kutosha, wakulima watalima misimu mitatu kwa mwaka hivyo kuongeza pato la familia na Taifa kwa ujumla. 

Akizungumza kabla ya uzinduzi wa mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. William Mwakilema amesema kilimo cha umwagiliaji ni kilimo cha uhakika na kwamba mradi huo utawanufaisha wakazi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.    

Aidha Mhe. Mwakilema amezitaja faida nyingine zitokanazo na mradi huo pamoja na kuepusha athari za mafuriko yanayowasababishia hasara wakulima ikiwemo mbegu zilizopandwa shambani kusombwa na maji ya mafuriko, sanjari na hayo Mwakilema amesema bwawa hilo pia litachangia kuwepo kwa shughuli zingine za kiuchumi ikiweno uvuvi wa samaki.      

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa amewaasa wananchi wa Korogwe kushiriki katika ulinzi wa vifaa vya ujenzi na kuepuka vitendo vya wizi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanahatarisha shughuli za ujenzi wa bwawa hilo.       

Ujenzi wa bwawa hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa  mwezi wa saba mwaka 2025 ambapo bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo milioni mia mmoja (100), ambapo baadhi ya skimu zitakazonufaika na bwawa hilo ni pamoja na Skimu ya Mkameni, Mombo, Chekelei, Kwemkumbo, Mkomazi Juu na Magila Gereza.

Post a Comment

Previous Post Next Post