Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji iongeze kasi katika uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua pamoja na kujengeni mabwawa ya kukinga maji ili yatumike wakati wa kiangazi, kwenye ukame na kuzuia mafuriko.    


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Kusimamia Rasilimali za Maji nchini, kwenye ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Februari 11.2024 ambapo Waziri Mkuu alikua mgeni rasmi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza viongozi wa Bodi za Maji wa Mabonde waongeze jitihada katika uhifadhi wa vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kutangaza maeneo hayo kwenye gazeti la Serikali kama maeneo tengefu ili kuyalinda kisheria. 

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Februari 11, 2024) baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Taifa la Sekta Mtambuka kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Rasilimali za Maji katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  

“Bodi za Maji za Mabonde zitekeleze agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti Rafiki wa Maji katika Vyanzo vya Maji nchini iliyofanyika Tarehe 16 Novemba 2022 kwa kupanda  angalau miti rafiki wa maji  milioni 2.5 kwa mwaka.”  

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini zijenge na kusafisha miundombinu ya kusafirisha ama kuondoa maji ya mvua katika maeneo yao ili kuzuia mafuriko. “Wizara ya Madini idhibiti uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji kuhimiza wachimbaji kuzingatia utunzaji wa mazingira.”  

Kwa upande wa Wakala wa Misitu Tanzania, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wake wadhibiti upandaji wa miti mingi ya kibiashara katika vyanzo vya maji kwa kuwa miti ikikatwa eneo litabaki kuwa jangwa, piasuala hilo litekelezwe sambamba na kusitisha kutoa vibali vya kuvuna misitu kwenye vyanzo vya maji.  

Awali, Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika ujednzi wa miradi wa maji, ambapo amesema ulindaji wa rasilimali za maji utaendelea kupewa kipaumbele nchini.  

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikabidhi Tuzo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watanzania Pamoja na kuwa Kinara katika kusimamia Utunzaji na uimarishaji wa vyanzo vya maji, kwenye Hafla ya Ufunguzi wa Jukwaa la Wadau wa Sekta Mtambuka Katika Kusimamia Rasilimali za Maji Nchi, iliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Februari 11. 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambaye ameongea kwa niaba ya mawaziri wa kisekta amesema wataendelea kushirikiana kuhakikisha kwa pamoja wanazilinda rasilimali za maji.

Post a Comment

Previous Post Next Post