Serikali  inaendelea na utekelezaji wa shughuli za usafi wa Mazingira na uboreshaji wa  miundombinu ya matundu 100  ya vyoo katika shule zilizokuwa zikitumika kuhifadhi  waathirika wa maporomoko ya udongo wilayani Hanang Mkoani Manyara. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa afua mbalimbali zenye lengo la kurudisha hali katika uhalisia wake. Uboreshaji wa vyoo katika Shule hizi unasaidia kuweka utayari wa mazingira safi pindi shule zitakapofunguliwa Mwezi Januari.


Mkuu wa Sehemu ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima akizungumza katika zoezi la ukarabati wa matundu 32 ya vyoo shule ya Msingi Gendabi amesema uwekaji wa matundu  ya vyoo ya kisasa utasaidia wanafunzi kufurahia Mazingira ya kujifunzia kutokana na ubora wa vyoo hivi ambavyo hutumia maji kidogo na hudhibiti  harufu mbaya pamoja na wadudu .

“Vyoo vilivyokuwepo vilikuwa na mapungufu kadhaa ambayo tumebaini hivyo, tumeamua kuboresha ambapo kutakuwa na faida nyingi ikiwemo utumiaji wa maji kidogo, hakutakuwa na harufu mbaya, wadudu kama mende hawatakuwepo na hofu ya kutumbukia haipo hata mtoto anayetambaa hawezi kutumbukia ,pia wadudu hatarishi kama nyoka hata akitumbukia hataweza kutoka tena maana kina mfuniko unaojifunika”amesema.
 

Aidha ,  Mwakitalima  amewahakikishia  Wazazi kuwa baada ya kambi kufungwa Mazingira ya shule ni salama kwani tayari wameshanyunyizia dawa kuondoa  wadudu na mazingira yanakuwa bora zaidi kuliko awali.

Naye Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara  Editha Jonathan amesema usafi wa mazingira na ukarabati wa miundombinu ya vyoo utasaidia kuepuka magonjwa ya mlipuko huku akisema usambazaji wa jumbe za uelimishaji kuhusu masuala ya afya umekuwa ukiendelea.
 

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Shule ya Msingi Gendabi Mwalimu Kindoli Twaha ameshukuru hatua hiyo ya uboreshaji wa miundombinu ya matundu ya vyoo.

“Maboresho haya tunayafurahia sisi kama walimu maana  mwanafunzi hawezi kuona tundu la choo na vinatumia maji kidogo sana”amesema.
 



Post a Comment

Previous Post Next Post