WANANCHI wa mkoa wa Iringa wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kuchangia maoni ya utayarishaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Halima Dendego akifungua hafla ya wadau wa mkoa wa Iringa walioshiriki katika warsha ya siku moja ya uhamasishaji wa wadau kushiriki katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akifungua mkutano wa Uhamasishaji wa Ushiriki wa wadau katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bibi. Halima Omari Dendego ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali wa mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuchangia maoni yao ya nini wanahitaji kifanyike katika miaka 25 ijayo.

Amesema hadi sasa, maendeleo yaliyopo ni muongozo bora uliokuwepo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo utekelezaji wake unakaribia kukamilika.

“Taifa letu limepiga hatua kubwa katika maendeleo kutokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo itafikia tamati mwaka 2025; tunapaswa kuandaa muongozo mwingine ambao ndio utakuwa dira yetu ya kuelekea kwenye maendeleo makubwa zaidi ya haya tuliyoyafikia kwa miaka 25” amesema Bibi Halima Dendego

Bi. Dendego ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kuwa huru kutoa maoni yao wakati utakapofika wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya utayarishaji wa Dira hii ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Dkt. Linda Salekwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi akichangia hoja wakati wa hafla ya uhamasishaji wa wadau kushiriki katika uchangiaji wa maoni wakati wa uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizugumza kwa niaba ya timu ya Uhamasishaji wa wadau kushiriki katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Dkt. Joel Silas amesema lengo la uhamasishaji huu ni kuwandaa Watanzania kushiriki kimamilifu katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kutoa maoni yao wakati utakapofika.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wananchi katika makundi yote ndani ya jamii ili watoe maoni yao wanataka Tanzania ya miaka 25 ijayo iweje na iwe na hatua gani ya maendeleo.

Wadau mbalimbali wa Iringa wakifuatilia wasilisho wakati wa warsha ya uhamasishaji wa wadau kushiriki katika uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dkt. Silas amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2000 imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuiwezesha nchi kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kipato cha kati na Maisha bora kwa watanzania.

Aidha, ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana katika miaka 25 iliyopita kuwa ni pamoja na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wastani wa zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka katika kipindi chote cha utekelezaji wa dira, upatikanaji wa huduma bora za kijamii kama maji, elimu na miundombinu bora ya usafiri na usafirishaji na huduma zingine.

Kamati ya unandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 wakifuatilia hoja za wadau kuhusu mchakato wa uandishi wa dira hiyo katika hafla iliyofanyika mkoani Iringa.

Mchakato wa utayarishji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ulizinduliwa rasmi tarehe 03 Aprili 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango. Kwa sasa, Serikali inaendelea na uhamasishaji wa wananchi kujiandaa kutoa maoni yao ya kutayarisha dira hiyo.

   


Post a Comment

Previous Post Next Post