Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewasilisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2023 Bungeni Jijini Dodoma ikiwemo Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa, Sura ya 419 ambapo pamoja na mambo mengine marekebisho haya yanakusudia kutoa mamlaka kwa Rais kutangaza tarehe ya maziko ya Rais aliyefariki akiwa madarakani kuwa ni siku ya mapumziko.
“Sehemu ya Tano ya Muswada inapendekeza marekebisho kwenye Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa, Sura ya 419 ambapo kifungu cha 6 kinapendekezwa kufutwa na kuandikwa upya kwa lengo la kuboresha masharti kuhusu mamlaka ya Rais kutoa tangazo la kifo cha Kiongozi wa Kitaifa au Kiongozi mahsusi aliye madarakani”
“Marekebisho hayo pia yanampa mamlaka Kiongozi mahsusi aliye madarakani kutoa tangazo la kifo cha Kiongozi mahsusi mstaafu, vilevile marekebisho haya yanakusudia kutoa mamlaka kwa Rais kutangaza tarehe ya maziko ya Rais aliyefariki akiwa madarakani kuwa ni siku ya mapumziko”
“Lengo la mapendekezo haya ni kuweka bayana na kutofautisha mamlaka zinazopaswa kutoa matangazo ya vifo vya Viongozi wa kitaifa na Viongozi mahsusi, vifungu vya 9 na 10 vinapendekezwa kurekebishwa ili kutoa Mamlaka kwa Kiongozi mahsusi aliye madarakani kutoa tangazo la kifo cha Kiongozi mahsusi mstaafu, lengo ni kutambua utaratibu unaotumika sasa ambapo pamoja na kwamba Sheria imemtaja Rais kama mamlaka ya kutoa tangazo la kifo cha Kiongozi mahsusi mstaafu, matangazo ya aina hiyo kwa kawaida yamekuwa yakitolewa na Viongozi mahsusi walio madarakani”
Post a Comment