Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma, (Mb) amesema Serikali ina lengo la kuingiza somo la Maadili kwenye Mtaala wa Elimu ili kukabiliana na Changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii. 

Naibu Waziri, Wizara ya Utamaduni, Sanana na Michezo, Hamis Mwinjuma 

Katika taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa instagram wa Wizara ya Utamaduni, Sanana na Michezo, Naibu Waziri Hamis Mwinjuma amesema hayo leo Aprili 18, 2023 Bungeni jijini Dodoma alipokua akijibu swali la Mhe. Bahati Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua ni lini Serikali italiingiza somo la Maadili kwenye mitaala ya Elimu. 

Mwinjuma amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra kwenye jamii kupitia vyombo vya Habari akibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2023 wizara imefanya vipindi 11, pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 wamefanya Vipindi 21 kwenye vyombo vya habari vya kijamii. 


"Kupitia Tamasha la pili la Utamaduni litakalofanyika Mei 19 hadi 21, 2023 mkoani Njombe, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo wamiliki wa vituo vya malezi, shule, midahalo na semina Maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini" amesema Mhe. Mwinjuma. 

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara yenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto, vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kutekeleza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na hali ya mmomonyoko wa maadili unaoendelea kujitokeza hapa nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post