Wizara ya afya imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa afya Ummy Mwalimu la kuhakikisha watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano wanapatiwa chanjo ya Surua mkoani Katavi   ambapo wataalamu kutoka wizarani  kwa kushirikiana na halmashauri  wanapita nyumba kwa nyumba kutoa huduma hiyo.



Na. Elimu ya Afya kwa Umma

Ikiwa ni siku mbili  zimepita tangu agizo hilo litolewe na Waziri wa afya Ummy Mwalimu akiwa ziarani mkoani Katavi katika halmashauri ya Mpimbwe  utekelezaji wake umeanza na  mwitikio wa wazazi kuwapeleka watoto kwenye chanjo  ni mkubwa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya afya kwa umma kutoka Idara ya Kinga Wizara ya afya Dkt. Tumaini Haonga amesema mbali na chanjo hiyo kuanza kutolewa Mpimbwe, maandalizi ya kampeni kwa ajili ya  halmashauri ya Tanganyika na Mlele yamekamilika.

Aidha ,Dkt. Haonga amesema  kampeni hiyo ya chanjo ya Surua inakwenda sambamba na magari ya matangazo yaliyotolewa kwa ajili ya elimu na uhamasishaji wa chanjo ya Surua.

“Haya magari 10 ya matangazo ni maelekezo ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu aliyoyatoa wakati anafanya zoezi la uzinduzi maalum la utoaji wa elimu ya afya kwa umma, uhamasishaji na utoaji wa chanjo  dhidi ya Surua  katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe  tunaenda na kampeni ya “Mtu ni Afya bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo mbalimbali pamoja na chanjo ya Surua wanajitokeza kupata chanjo na zoezi hili litatekelezwa kwa mwendelezo wa siku 14”amesema Dkt.Haonga.

Dkt. Haonga amesema magari hayo ya matangazo yataifikia jamii kwa ukamilifu kwa sababu yatakuwa na wataalam.


“Pamoja na kutoa ujumbe maalum uliorekodiwa kuhusu masuala maalum ya afya hususan ujumbe wa Surua, magari haya pia yatakuwa na mhamasishaji mmoja kwa  kila gari ambapo kunakuwa na mhudumu wa afya ngazi ya jamii, pamoja na wataalam wa afya kutoka vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na wataalam kutoka wizara ya afya. “amefafanua Dkt. Haonga.

Pia, Dkt. Tumaini amesema wanashikisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na waganga wa Tiba Asili kuwa na uelewa wa pamoja katika kuhakikisha elimu inafika kwa kila mtu.

Katika kampeni hiyo, Dkt. Haonga  amehimiza ushirikiano katika zoezi hilo na kutoa wito kwa viongozi  serikali za mitaa kuwa mstari wa mbele kuwezesha wananchi kuweka mazingira rahisi ya usafi katika kujikinga na magonjwa mbalimbali.

“Tuendelee kuzingatia kanuni za afya,kuzingatia usafi binafsi, ili kufanikisha vizuri nitoe wito kwa watendaji na wenyeviti kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi ili wawe na afya bora ”amesema Dkt. Haonga.

Wakizungumza  katika utekelezaji wa zoezi hilo,  baadhi ya wakazi wa Chamalendi halmashauri ya Mpimbwe wamesema wengi wao wamefahamu umuhimu wa Watoto kupata chanjo hiyo.

Magdalena Kulwa ni mkazi kijiji cha Mwamabambasi kata ya Chamalendi Halmashuri  Mpimbwe  Wilayani Mlele Mkoani Katavi  ambapo amesema ameitikia hamasa hiyo baada ya kuleta watoto saba wa familia moja kupata chanjo hiyo.

Amesema ugonjwa wa Surua sio wa kufanyia mzaha ndio maana wao kama familia wameamua kuwakusanya watoto wote 7 wa familia moja wakiwemo watoto watoto wake wawili kupata chanjo  kwani kuanzia sasa wameujua ukweli baada ya  kusikia kampeni ya Chanjo kupitia matangazo ya kwenye magari.

“Nawaambia na wengine wawalete wapate chanjo wasiwapeleke kwa Waganga wa Tiba Asili, nimetoka kazini nimewaleta kuna ugonjwa mkali sasa hivi, ugonjwa huu sio wa kuwapeleka kwa Waganga ”amesisitiza Magdalena.

Naye Ashura Maganga  ni mama  mwenye mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye alijifungulia maporini na kusaidiwa na wasamaria wema anasema hitaji lake kuu kwa sasa ni chanjo ya Surua .

“Nahitaji chanjo ya Surua  nilijifungua porini kwa shida sitaki kumpoteza mtoto wangu kwa sababu ya Surua, tangazo nimesikia tu kwenye gari na nilikuwa sina uelewa wowote kuhusiana na chanjo nawashauri na wenzangu watumie fursa hii ya chanjo”amesema Ashura.

Bahati Lulyalya ni mmoja ya wananchi wa Chamalunde pia  ambaye alishindwa kujizuia kuelezea hisia zake baada ya kufurahishwa na hatua za Wizara ya Afya  kuwafuata mahala walipo.

“Nashukuru sana Wizara ya Afya kwa kutufikishia hii huduma, mpaka nimejua kuwa Surua ni ugonjwa mbaya sana dalili zake huonekana kwa upele  mdogomdogo na macho kuwa mekundu nashauri watoto wawahishwe sana kwenye huduma maana Wizara ya Afya wapo hapa kwa ajili ya kutusaidia”amesema Bw. Lulyalya.

Naye Mganga Mfawidhi  zahanati ya Chamalendi   Abdul Musa eneo  lililoathiriwa na ugonjwa huo amesema  wanapokea wagonjwa wa lika tofauti.

 

Ikumbukwe kuwa awamu ya kwanza zaidi ya Watoto laki mbili watapata chanjo hiyo mkoani Katavi  na zoezi hilo litakuwa endelevu ili kuboresha afya za watoto huku serikali kupitia wizara ya afya imeongeza msukumo wa utoaji wa elimu na uhamasishaji wa chanjo ya Surua katika mkoa wa Katavi  kwa kutoa magari ya matangazo kwa ajili ya uhamasishaji ambapo hamasa  imeshaanza kuzaa matunda  baada ya wananchi kuanza kujitokeza  kuwapatia watoto chanjo huku wakiiomba serikali kuongeza chanjo.

Post a Comment

Previous Post Next Post