Serikali imezindua Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Dawati la kutokomeza Ukatili wa Kijinsia katika maeneo ya Umma ili kuwasaidia wananchi kwenye maeneo hayo  kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Dawati la kutokomeza Ukatili wa Kijinsia katika maeneo ya Umma uliofanyika Februari 17, 2023 eneo la soko la Mbuyuni, mkoani  Kilimanjaro.

Na Mwandishi Wetu

Akizindua Mwongozo huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, katika soko la Mbuyuni wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro Februari 17, 2023 ameitaka Jamii kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili kupitia Kamati za ulinzi wa Wanawake na watoto kwenye maeneo yao.
 
Waziri Dkt. Gwajima amesema Mwongozo huo ni wa kila mdau ambaye anatekeleza ajenda ya Serikali ngazi zote yaani kuanzia wananchi wenyewe, viongozi wa Serikali ya mtaa au kijiji, watendaji wa Kata na Halmashauri na hata wanasiasa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Moshi, mkoa wa Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Dawati la kutokomeza Ukatili wa Kijinsia katika maeneo ya Umma uliofanyika Februari 17, 2023.

"Natarajia kila mdau ataona umuhimu wa kusoma na kutekeleza mpango wa ufuatiliaji ulioelezwa kwenye Mwongozo huu kwani utahusisha taarifa za mikoa kuwasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI na kisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ambapo itampelekea Waziri Mkuu ambaye, Ofisi yake ndiyo inaratibu masuala yote ya kisekta ya kupambana kutokomeza Ukatili wa Kijinsia" amesema Dkt. Gwajima.

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amehimiza Mwongozo  huo kunasambazwa kila mkoa kwa kushirikiana na Wizara katika  Ili kuanzisha Madawati hayo katika maeneo ya Umma.

Mhe. Dkt  Gwajima ameongeza kwamba, anatambua Jamii ina vipaumbele vingi ikiwemo Elimu, afya, maji, umeme, Bararara ambavyo vinavyojadiliwa kwenye vikao vya kata na vijiji na kusisitiza kuwa ajenda ya kuwalinda watoto na Wanawake iongezwe pia katika ajenda hiyo iwe ya Kudumu.

Aidha ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kuzielekeza mamlala za Serikali za Mitaa kuweka Sheria ndogo na kufanya ajenda ya ukatili kuwa ya Kudumu kwenye vikao vyote vya maamuzi. 

"Tukaisimike ajenda hii kwenye vikao vyote, kutoijadili ni kama kuvibariki vitendo hivi kuendelea" ameongeza Waziri Gwajima.

Hali kadhalika, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Mwongozo huo ni sehemu tu ya mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo wananchi wote washirikiane kuanzia ngazi ya familia kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Akitoa salam za Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori amesema mkoa unaendelea kushirikiana na wadau kutokomeza vitendo vya ukatili kwa kutekeleza mipango na miongozo yote inayotolewa.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Linus Kahendaguza amesema Ofisi hiyo ina jukumu la kutekeleza Mwongozo huo kupitia watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na tayari imeshaelekeza kutungwa kwa Sheria ndogo za kudhibiti vitendo vya ukatili kwenye maeneo ya Umma.

Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni, Wilaya ya Moshi, mkoa wa Kilimanjaro  wakifuatilia uzinduzi wa Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Dawati la kutokomeza Ukatili wa Kijinsia katika maeneo ya Umma wakifuatilia matukio wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji  wa dawati la Jinsia kwenye maeneo ya Umma, uliofanyika sokoni hapo, Februari 17, 2023 Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro

"Wanawake wana haki ya kujumuika kwenye mikusanyiko mbalimbali kwenye Jamii lakini sehemu hizo mara nyingi Wanawake wanadhalilishwa hivyo Mwongozo huu utasaidia
kupunguza au kumaliza kabisa mashambulio ya aibu"  amesema Kahendaguza.

Naye Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali linalojihusisha na kupinga ukatili wa kijinsia la EQUALITY FOR GROWTH(EFG) Bi. Jane Magigita amesema chimbuko la kuandaliwa kwa Mwongozo huo ni utafiti uliofanywa katika baadhi ya mikoa nchini na kubaini changamoto ya udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa Wanawake kwenye maeneo ya Umma.

"Kwa kuanzisha madawati katika maeneo ya Umma, naamini kwamba masoko yetu maeneo ya Michezo,vituo vya mabasi, maeneo ya uvuvi na mengine kama bustani za wazi yatakuwa maeneo salama kwa Wanawake na wanaume watakaoyatumia" amesema Bi. Jane 


Kwa upande wao wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni kupitia Mwenyekiti wa soko hilo Bw. Lameck Mziray amesema kesi za watoto kunyanyaswa zimefika na wamechukua hatua na kuzifanyia kazi hivyo Mwongozo huo umefika kwa wakati muafaka.

Post a Comment

Previous Post Next Post