YOUR FUTURE IS CREATED BY WHAT YOU DO TODAY, NEVER TOMORROW





Na Elizabeth Msagula

Watafiti kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salam kwa kushirikiana na Idara ya Malikale wamesisitizwa kuendelea kufanya tafiti katika eneo la Tendaguru Manispaa ya Lindi yalipogundulika masalia ya mjusi mkubwa (Dainosaria) yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani ili kubaini endapo kuna masalia zaidi au aina nyingine ya Mijusi inayofanana na hiyo. 

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozuru katika eneo hilo jana Januari 9,2023 amesisitiza kuwa, "haiwezekani tuishie kuwatambua viumbe walewale tangu walipogunduliwa na Wajerumani, tuendelee kufanya utafiti kila siku kama ambavyo nchi ya Egypt inavyoendelea kugundua vitu mbalimbali, na sisi lazima tufanye watakuwepo wengine" 

Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amepotembelea eneo hilo la Tendaguru kuona kazi ya utafiti inayofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa nchini Tanzania. 



Wajerumani walifanya tafiti katika eneo hilo la Tendaguru na kugundua mabaki ya mifupa ya Dainasoria huyo mnamo mwaka 1908, hivyo Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameona ni vyema watafiti wakaendelea kufanya tafiti zao ambazo wamezianza na kugundua masalia mapya na kwa kufanya hayo, watagundua masalia mengi zaidi ambayo yanaweza kutunzwa na kuwa kivutio kikubwa cha utalii na Taifa. 


Awali Mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini Tanzania Dkt. Noel Lwoga ameeleza kwamba, kwa hatua ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na utamaduni UNESCO Disemba 2022 kulitambua eneo la Tandaguru kama sehemu ya urithi wa Dunia, kwa matazamio kunatoa picha na imani kuwa miradi mikubwa ya utafiti itakayowezeshwa na shirika hilo inaweza kufanyika na eneo hilo kuendelezwa vizuri. Hata hivyo alishukuru ushirikiano ulipo kati ya Chuo kikuu cha Dar Es salaam na Makumbusho ya Taifa kwani utaleta tija kubwa kwenye suala zima la utafiti na kuliendeleza eneo hili la Tendaguru. 


Katika ziara hiyo Dkt. Jakaya Kikwete ametembelea eneo la Mkwajuni kinapojengwa kituo cha Kutolea taarifa kabla ya kufika eneo la Tendaguru ambapo kituo hicho kitakuwa na eneo la Ofisi, Bohari ndogo, Maonesho na sehemu ya kufanyia utafiti. Pamoja na kutazama eneo la chuo Kikuu cha Dar es Salam patakapojengwa tawi la chuo hicho litakalojihusisha na kilimo.


Naye Kaimu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar Es salaam Prof. William Anangisye amesema, Chuo kikuu kiko tayari kushirikiana na Makumbusho kwenye suala zima la utafiti na kusema wameshatenga fedha, tayari kwa kuanza kufanya utafiti.

Post a Comment

Previous Post Next Post