Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeipinga kauli ya kiongozi wake wa zamani, Nape Nnauye aliyesema ushindi katika uchaguzi hautokani na wingi wa kura za kwenye boksi, bali nani anayehesabu na kutangaza matokeo.


 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla leo Jumanne Julai 16, 2024 amesema kauli hiyo haitokani na msimamo wa chama hicho.

 

“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambia hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” amesema.

 

Kwa mujibu wa Makalla, chama hicho kitaheshimu matokeo yoyote na uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura.

 

“CCM itaheshimu matokeo yoyote na uamuzi wowote wa wananchi kupitia sanduku la kura na yeyote atakayeshinda kwa haki ndiye atakayepewa ushindi,” amesema Makalla

 

Awali, Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, alitoa kauli hiyo jana usiku Julai 15, 2024 alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi.



Katika kuwahakikishia ushindi wa mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Nape ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema: “Unajua ninyi sikilizeni, matokeo ya kura siyo lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi tu mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea.”


TAZAMA VIDEO HAPA CHINI;

 


Post a Comment

Previous Post Next Post