Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani imefanya kikao cha wadau wa Afya Moja katika kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kuanzia tarehe 13 Disemba Hadi tarehe 15 Disemba 2023 Mjini Morogoro. 

 

 

Kikao kimekutanisha Wadau kutoka Wizara ya Afya na Wizara mtambuka na Taasisi  kama vile (Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu, Maji, Kilimo, Mifugo, Elimu) Taasisi za Utafiti, Vyuo Vikuu, na Wadau wa Maendeleo

 

Kikao kililenga kufanya uchambuzi wa awali (situation analysis) wa mbinu ya Afya Moja katika kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele hasa yale yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. 

 

Akifungua Kikao hicho Dkt. Tumaini Haonga ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga amesema

 

"Tanzania inajivunia kuanzishwa kwa Kurugenzi  Maalum ya Uratibu wa Afya Moja  ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, yenye lengo la kuoanisha afua katika Wizara zote ili kudhibiti Magonjwa yanayohitaji ushirikishwaji wa Sekta mbalimbali. 

 

Zaidi ya hayo, amesema Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP), ulianzishwa mwaka 2009 chini ya Wizara ya Afya ili kuweza kuratibu Magonjwa haya. 

 

Hata hivyo, licha ya juhudi hizi zilizoratibiwa, bado Magonjwa ya NTDs hasa yanayoambukizwa kutoka wanyama kwenda kwa binadamu yanaendelea kupokea uangalizi duni kutoka kwa mifumo ya huduma za afya, taasisi za utafiti, Elimu na watunga Sera"amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post