YOUR FUTURE IS CREATED BY WHAT YOU DO TODAY, NEVER TOMORROW

Serikali imetakiwa kulipa fidia ya dola 109 milioni (Sh260 bilioni) kwa Kampuni ya Indiana Resources iliyoshinda kesi katika Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID) baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.  


Kwa mujibu wa taarifa iliyosambaa mitandaoni, hukumu hiyo iliyotolewa Julai 14, mwaka huu, ambapo Tanzania imetakiwa kulipa fidia ya dola 76.7 milioni, sanjari na riba ya asilimia mbili iliyokokotolewa kuanzia Januari 10, 2018 baada ya kufunguliwa kesi hiyo, hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa dola 109.5 milioni (sawa Sh260 bilioni kwa sasa).  

"Kiasi cha tuzo hii kinaonyesha uwekezaji mkubwa ambao umepotezwa na wanahisa baada ya Serikali kutwaa Ntaka Hill kinyume cha sheria," amenukuliwa Mwenyekiti Mtendaji wa Indiana Resources Bronwyn Barnes katika taarifa yake kwa umma baada ya hukumu hiyo.  

Mgogoro huo unachagizwa na marekebisho ya Sheria ya Madini ya 2017, ambayo pamoja na mambo mengine, ilifuta misingi ya kisheria ya umiliki wa leseni ya kuhodhi eneo la madini katika kipindi cha tahadhari ya biashara ya madini hayo katika soko, ili kulinda mtaji wa mwekezaji (Retention Licenses).  

Januari 10, 2018, Serikali ilichapisha kanuni za Madini (Haki za Madini), ambapo chini ya kanuni ya 21 ya kanuni hizo, Serikali ilifuta leseni zote za kuhodhi ardhi zilizotolewa kabla ya tarehe 10 Januari 2018.  Leseni hizo zilikoma kuwa na athari yoyote ya kisheria. 

Haki za maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na leseni iliyokuwa kwa Indiana Resources zilihamishiwa kwa Serikali.  Kwa mujibu wa Indiana iliyokuwa ikimiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili za Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited, zilijaribu kuishawishi Serikali kurejesha leseni hiyo lakini haikufanikiwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 ndipo ikawasilisha ombi la fidia ICSID.  

Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano ya mkataba wa Uwekezaji wa Tanzania (BITs) kati ya Tanzania na Uingereza chini ya uwekezaji wa kampuni hizo mbili za Uingereza.

Post a Comment

Previous Post Next Post