Wahariri wa vyombo vya habari vilivyopo ndani au pembezoni mwa shoruba za Kwakuchinja, Amani-Nilo na Nyerere Selous-Udzungwa wameazimia kupambana na uharibifu wa bioanuwai na mabadiliko ya tabianchi, hatua itakayosaidia kuilinda dunia kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

 

Na Alfred Mlonganile.

Azimio hilo lilifikiwa Disemba 12, 2023 baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wahariri hao namna ya kuripoti habari za bioanuwai ikijumuisha maisha ya viumbehai (wanyama na mimea) na mifumo ya maisha yao.

“Haya mafunzo yamenipa mwangaza mkubwa na mwangaza huo hautofia kwangu, nitahakikisha naenda kuacha alama katika kituo changu ili tusaidiane katika hii kazi. Na timu hii itachangia kuleta matokeo chanya kwa jamii tutakayohakikisha inafahamu umuhimu wa utunzaji wa bioanuwai”. Khatibu Salim Omary – Mhariri Nuru Fm, Tanga.

“Wanahabari tumekuwa hatuna uelewa mzuri wa namna ya uandishi wa habari za bioanuwai hivyo mafunzo haya yatasaidia kuandaa kazi zetu kwa kina ili kupambana na uharibifu wa maliasili tofauti na ambavyo tumekuwa tukiandaa vipindi vya burudani zaidi na kuandika taarifa za mazingira pekee”. Hawa Rashid – Mhariri Manyara FM

Wahariri katika mafunzo ya uhifadhi Bioanuwai 

Miaka ya hivi karibuni ulimwengu umeshuhudia mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na uharibifu mkubwa wa biaonuwai ikiwemo ukataji wa miti hovyo na uzalishaji wa hewa ukaa.

Mabadiliko hayo ya tabianchi yameathiri watu na viumbehai wengine wakiwemo wanyamapori katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.

Joto linaongezeka kwa kasi barani Afrika katika miongo ya hivi karibuni na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuwa mbaya kwa mujibu wa ripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyozinduliwa Jumamosi Disemba 8,2023 kwenye mkutano wa Umoja Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 huko Dubai.

Pia ripoti hiyo imeeleza kuwa, takribani dola trilioni 7 za fedha za umma na za sekta binafsi kila mwaka zinatumika kusaidia shughuli zenye athari mbaya kwa mazingira zinazochochea moja kwa moja mabadiliko ya tabianchi pesa ambayo ni mara 30 ya kiasi kinachotumiwa katika ufumbuzi wa suluhu za mazingira kila mwaka

Kando ya Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) la 2023 lililofanyika Disemba 3 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumejadiliwa namna ya kushughulikia masuala ya bioanuwai kwa vijana ambapo walimu na waelimishaji 400 kutoka nchi 90 walijiunga na mazungumzo hayo.

Nchini Tanzania, serikali imewekeza juhudi kubwa kupambana na uhalibifu wa bioanuwai ikiwa ni pamoja na kuwaandaa askari wa maliasili wanaopambana na ujangili na ukataji misitu hovyo, kuanikiza upandaji wa miti na kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika mbalimbali kufadhili mafunzo ya uhifadhi wa maliasili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) - 2023 

Hii imetoa nafasi kwa wadau kushiriki katika juhudi za makusudi za kulinda biaonuwai ikiwemo Nukta Africa ambao wametumia jukwaa hilo kukutana na wanahabari kwa kutambua nguvu ya mawasiliano katika vita hii.

Katika mafunzo ya siku mbili, yaliyofanyika jijini Tanga, kuanzia tarehe 11 – 12 Disemba 2023 yaliyoandaliwa na Nukta Africa kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wake wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa wahariri wa vyombo vya habari, imeangaziwa umuhimu wa kujenga ufahamu na kuwashirikisha vijana na watu wenye mahitaji maalum katika kuchukua hatua kwa ajili ya biaonuwai, na jinsi ya kuwapa taarifa za kuaminika wawapo shuleni na katika maisha ya kila siku ili wafahamu kuwa hii ni tunu na inapaswa kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

“Tutahakikisha kuwa hiki tulichokipata inakuwa lulu na tunatunza ili kuwarithisha vizazi vijavyo. Pia hii ni tunu ambayo tusipoitunza inaweza kupotea hivyo tunaahidi kuendelea kuihamasisha jamii kulinda biaonuwai”. John Mbaga – Mhariri Rumeni FM Radio.

Wahariri katika mafunzo ya uhifadhi Bioanuwai

Wanahabari hao aidha wamehimizwa kuandaa Habari za kiuchunguzi ambazo hutegemea zaidi tafiti na ukusanyaji wa takwimu na kuongezewa ujuzi juu ya awasilishwaji wa taarifa za takwimu ili kufikisha taarifa zilizokusudiwa kwa jamii husika kulingana na mahitaji.

Licha ya uhaba wa rasilimali hasa rasilimali fedha ambayo imekuwa changamoto kubwa katika utekelezwaji wa mikakati mikubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda biaonuwai katika nchi zinazoendelea, serikali za mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania imeendelea kuwekeza katika miradi ambayo ni mbadala wa matumizi ya kuni na uzalishaji wa hewa ukaa mfano uzakishaji wa gesi na kuuzwa kwa bei nafuu.

“Kusambaza gesi asilia, kupunguza gharama za umeme, kuwezesha wananchi kutumia mitambo ya ‘Biogas’ ni jambo ambalo si rahisi kwa serikali kuamka asubuhi na kutekeleza hilo ama kuondoa kodi kwenye kila kitu.

Lakini kwa upande wa tasnia ya habari, tunao wajibu wa kuhakikisha tunawapatia wananchi taarifa, elimu na kuhakikisha tunapambana kubadilishwa kwa sera zitakazoenda kuandaa mkakati halisi wa utekelezwaji wa kulinda bioanuwai. Pamoja na hiki kidogo, ni lazima tuwe na namna ya kutekeleza mambo makubwa. Nuzulack Dausen – Mkurugenzi Mtendaji, Nukta Africa.                       

Inakadiliwa kuwa, sasa ulimwenguni kunatoweka viumbe hai wapatao 1,000 kwa mwaka ambayo ni mara 100 zaidi ya wakati wowote uliowahi kutokea katika historia ya mwanadamu hali inayoonesha hatari ya uharibifu wa maliasili na athari zake. Ni jukumu letu sote kulinda biaonuwai kwa ustawi wa maisha ya viumbe (mimea na wanyama) ulimwenguni. Bioanuwai, Rafiki Damu Damu

Post a Comment

Previous Post Next Post