Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine Dkt. Alexander Makalla amesema kijana Simon aliyejikata uume wake anao uwezo wa kupata mtoto endapo ana uhitaji huo. 

Dr Makalla ametoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari waliofika hospitalini hapo kufahamu hali ya kijana huyo ambapo amesema, kutokuwepo kwa uume hakuwezi kumuathiri katika maisha yake ya kawaida kwani anaweza kupata hisia isipokuwa atakosa kushiriki tendo la ndoa ingawa anaweza kupata mtoto bila kufanya tendo hilo. 

Amesema mfumo wa uzazi umegawanyika katika sehemu kuu mbili (mfumo wa uzazi wa ndani na nje) na kwa mwanaume, mfumo wa uzazi wa nje unahusisha uume na korodani ambapo korodani zinazalisha mbegu za kiume na kwa sasa kuna uwezekano pia wa kuvunwa mbegu za kiume kwake na kupandikizwa mwenza wake kwakuwa mbegu za kiume bado zinaendelea kuzalishwa. 

Kuhusu kupandikiza uume ameeleza kwamba anaweza kufanya hivyo kwa kuwekewa uume wa bandia endapo kama atakuwa na uwezo kifedha. Akieleza hali ya mgonjwa, mganga huyo mfawidhi wa hospitali ya Rufaa mkoa wa Lindi Dkt. Makalla amesema licha ya mgonjwa kuanza kuongea na kutembea, bado wauguzi na wataalamu wa magonjwa ya akili wanaendelea na matibabu kuhakisha afya yake ya akili inakaa sawa na kwamba hawawezi kumruhusu mgonjwa huyo kurudi nyumbani mapema kwa kuhofia akirudi nyumbani anaweza kuendelea kujidhuru zaidi. 

Awali alipohojiwa juu ya kilichotokea alikiri kujidhuru mwenyewe kwa kutumia kisu butu akidai kuwa hayo ni Maelekezo  ambayo amekuwa akipewa kutoka juu na kwakuwa yeye ni mfalme mwaminifu, anatekeleza maagizo hayo. 

Ameongeza kuwa, wakati huu amewekewa mpira kwaajili ya kumsaidia kupata haja ndogo na kupona majeraha yake vizuri asipate maambukizi kwenye kidonda na baada ya wiki mbili mpira huo utatolewa na hivyo atakuwa yupo sawa.

Post a Comment

Previous Post Next Post